MFAHAMU MARION

Jina lake rasmi ni Marion Wanjiku. Ukimwita kwa jina lake la msimbo, Delta-Star, atafurahika Zaidi. Binti huyu ana umri wa miaka ishirini na minne (24).

Marion ni banati mwenye uzuri wa kupigiwa mfano. Si wajihi mwororo, si midomo mizuri, si macho ya kupendeza, si umbo la kuvutia, si moyo safi, si, si, si.

Safari yake ya masomo ilianzia kwenye shule ya msingi ya Al- Maktoum Academy, akasomea katika shule ya upili ya washichana ya State House na kisha kuukamilisha mfumo wa 8.4.4 katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Mombasa.

Ulemavu alio nao binti huyu ni tabasamu lisilonyauka. Hutabasamia yeyote na chochote mahali popote. Wingi wake huu wa tabasamu anakiri kuwa humwondolea manung’uniko ya kila sampuli.

Binti Marion amekoleza ukahawia wa ngozi. Kimo chake ni futi 5.6 na huvaa viatu vyenye ukubwa wa nambari sita. Kwa sasa hajadiriki kutojwa mwilini japo anatumai kufanya hivyo katika siku zijazo.
Makaazi yake ni mtaa wa Kitengela.

Badhi ya vitu anavyovipenda binti huyu ni;

 1. Kusafiri
 2. Kuogelea
 3. Kuandika Makala mtandaoni
 4. Kupika
 5. Kuwasaidia wasiojiweza

Marion anawachukia watu ambao humfanyia kinyongo bila ya kuwa na sababu mahususi, wenye kiburi, wenye majivuno na wachoyo.

Vyakula anavyovienzi ni;

 1. Pilau ya kuku
 2. Sima kwa mrenda
 3. Chai ya maziwa

Havipendi vyakula visivyo virutubishi kama vile pizza na burger.
Rangi anayoikumbatia ghashi huyu ni zambarau iliyokoleza. Kulingana naye, rangi hii huweza kuweka siri na vile vile huvutia sana.

Delta- Star anakiri kuwa angependa kuolewa na mwanamme mweupe mrefu. Katika ndoa yake hiyo, ana maono ya kupata wana wawili tu.

Kwa kuwa anapenda kutangamana na rafiki wapya, atafurahika ukimtafuta kwenye mitandao ya kijamii kama ifuatavyo;

 • Facebook- Delta Queensy
 • Instagram-marwanji

MSAMIATI

 • Kutojwa – kuwekwa tattoo

Je, unataka tutoe maelezo kukuhusu ili upate kujielewa vizuri, ufahamike vyema kwa rafiki zako, kuweka kumbukumbu mtandaoni na kupata rafiki wengine? Nitumie ujumbe kwenye:

 • 254729673536

ama

 • hussaynqassym@gmail.com

Shukrani za dhati kwa kusoma!

©husni

Advertisements

TIME TRAVEL~ USAFIRI WA NYAKATI

Laiti ningalikuwa na uwezo wa kusafiri na kurudi kwenye enzi zangu za awali, yapo mambo mengi ambayo ningaliyabadili. Ningeyabadili kwa pupa nikitegemea kuibadili Leo yangu na siku zangu za halafu.

La kwanza kubadili ingekuwa hali ya marehemu laazizi mamangu Aisha. Ningefanya kila juhudi kuhakikisha kuwa hali yake ya afya inabadili na kuwa shwari kabisa. Kwa ajili hii, asingeiaga dunia mapema hiyo.
Labda angekuwa hai hadi hii leo.

Mamangu Aisha angekuwa hai kumwona kifungua mimba wake akizidi kunawiri na kuwa mtu wa maana katika jamii. Binti Aisha angekuwepo kunipa shime na motisha ya kuzidisha ari yangu. Angekuwepo kuniliwaza wakati wa majonzi. Angekuwepo kunikosoa nikoseapo.

Labda nina yangu angekuwepo kumwona mke wangu na wanangu. Ningempeleka kuvinjari maeoneo ambayo hakufanikiwa kuyazuru katika ujana wake. Ningemnunulia zawadi na kumfurahikia siku zote. Angenivisha koja la maua kwenye hafla yangu ya mahafali na kunipongeza. Ningemwamini na siri zangu na kumwomba ushauri kila inapobidi. Labda angekipenda kiswahili changu na sauti yangu, kama alivyolipenda tabasamu langu.

Ila laiti itabaki kuwa laiti tu. Je, wewe ungepata fursa hii, ungebadili kitu kipi cha kwanza?

Shukrani.

©husni

EASTLINGTON CAFE

Biryani, pilau na mapochopocho ainati ya kufana utayapata hapa. Isitoshe, zipo sharubati tamu kupindukia na zenye ladha zote kama vile za machungwa, matikiti maji, mapapai, mananasi na hata ndizi pia.

Unaposikia kuhusu bei ya biryani, aghalabu uchu wa kukivamia chakula hiki hukutoweka ghafla. Hoteli, migahawa na mikahawa mingi huwa na bei za juu mno za kutamausha. Bila ya shilingi mia tano, kamwe huwezi kukata kiu yako ya biryani, ila mambo ni tofauti Eastlington. Ana bei za nafuu sana na ambazo bila shaka utafurahika kwazo. Kwa shilingi mia tu, utafaidi kutia mdomoni uhondo huu.Kwa taarifa yako, zipo ofa nyingi kwa wateja wajao Eastlington Cafe kama vile sharubati za bure.

Kwa wasio wenyeji wa Mombasa, basi mna pahali pa kupata burudani ya chakula kitamu na cha bei nafuu sana, endapo mtafika Mombasa kwa shughuli ama ziara. Mkahawa wa Eastlington ndipo!Mkahawa huu uko Kiziwi, Tudor, eneo bunge la Mvita, jijini Mombasa. Mpigie simu mwenye mkahawa huu, Khalid, kwa nambari +254726932633. Khalid ni mcheshi sana, mpenda watu na hufurahika kupata rafiki wapya. Huwenda akakualika kwa biryani ya bure ukimsemezesha vizuri.

Shukrani.

©husni

MFAHAMU BERYL

Mwite Beryl Achieng. Watu wa akraba yake wanalo jina maalumu wamwitalo kwalo, Manyanga. Beryl ni binti wa haiba na mwenye viwango vya juu vya kujifahamu, kujielewa, kujitambua na kujiamini. Ndio mwanzo ameabiri mashua ya miaka ishirini, ukipenda, yuko kwenye hatua za mwanzo za miaka ishirini (early 20’s).

Ghashi huyu ni mcheshi saa zote na huwa muhali sana kumpata akiwa amenuna. Miongoni kwa mavazi asiyokosa ni tabasamu la kuvutia. Anakiri kuwa hali hii humsaidia pakubwa kuzikabili hisia hasi kama vile majonzi, huzuni na hasira.

Beryl amekoleza weusi wa haja, huo ambao wengi wa adinasi hawajivunii kuwa nao. Anaipenda rangi ya ngozi yake wala hana nia ya kujichubua na kujipagaza weupe ghushi.

Huvalia viatu vya ukubwa wa nambari tano. Mwili wake haujathubutu kuchorwa wala hadhamirii kufanya hivyo maishani mwake. Si mbaguzi sana wa mifumo ya nywele. Hukubali mtindo wowote bora uwe wa kumchukua barabara na ambao unapikika chungu kimoja na uzito wa kibeti chake.

Banati huyu amesomea taaluma ya ualimu. Amebobea kwenye masomo ya kiingereza na fasihi, kazi anayoienzi sana. Kando na ualimu, Beryl amelivulia nguo suala la uandishi. Vile vile, mahaba yake kwa vitabu si ya kupigiwa mfano. Ni mwanachama wa vuguvugu la waandishi wa Mombasa (Writers Guild Mombasa) ambalo ni tokeo la vuguvugu la waandishi wa Kenya (Writers Guild Kenya), ambako waandishi ibuka hukuzana.

Baadhi ya vitu avipendavyo ni;
1) Kuvinjari mandhari
2) Vitabu
3) Mandhari ya bahari
4) Chakula
5) Kufundisha

Beryl anapenda sana vyakula vya wapwani. Anakiri kwamba watu hawa wana uchawi wao wa kuzigusa nyoyo ya walaji kwa hayo mapishi yao. Hula akaemewa kupindukia.

Hapendi chokoleti kwa kuwa huwa zamharibia ladha mdomoni.

Rangi anayokumbatia dada huyu ni samawati iliyokoleza. Kwake, rangi hii huashiria mrahaba (royalty).

Je, unataka tutoe maelezo kukuhusu ili upate kujielewa vizuri, ufahamike vyema kwa rafiki zako, kuweka kumbukumbu mtandaoni na kupata rafiki wengine? Nitumie ujumbe kwenye:

 • 254729673536

ama

 • hussaynqassym@gmail.com

Shukrani za dhati.

©husni

MFAHAMU ANANGWE

Jina lake ni Joshwa Victor Anangwe japo rafiki zake wa karibu wamempagaza Akalunji Papa, jina ambalo limekita tokea ukembe wake. Dume huyu anapiga mbizi kwenye maji makuu ya umri wa miaka thelathini.

Kimo chake ni futi 5.5 nalo tambo la mwili wake ni la kadiri, halijaegemea uneneni wala si kwamba halina udole. Ngozi yake, rangi ya kahawia nacho kiatu kinachomchukua barabara ni cha ukubwa wa nambari arobanne na tatu (43). Ghulamu huyu hatii madoido kichwani anaponyolewa, ila huhitari kuzilengeta katika mfumo wa urasimu ambao humpa mwonekano mzuri na maridadi.

Victor hupenda sana kutangamana na watu bila kubagua dini, umri, kabila ama kitembo cha elimu. Ucheshi wake huelekea kumfanikishia huko kutangamana na watu. Ana huba ya dhati kwa vazi tai. Mara nyingi, hupenda kuvaa tai iwe kazini, kanisani, mikutanoni ama popote panapostahili kuvutia, jambo ambalo limemtia matatani Mara si moja anapojipata kitandani na vazi hili. Vile vile, hakosi kuvalia suti walau Mara mbili ama tatu kwa juma.

Makaazi yake no viunga vya mji wa kakamega. Kitaaluma, Anangwe ni mwana isimu wa lugha (Linguist) na mwandishi mahiri (African Linguistic Enthusiast). Ameandika kitabu ‘Tsindalo Tsia Abaluhyia’ ambacho anapania kuchapisha katika siku chache zijazo.

Kwa sasa, ni msimamizi wa hospitali mojawapo kwenye gatuzi la Kakamega.

Alisomea kwenye shule ya msingi ya Eshiakhulo, akajiunga na shule ya upili ya seminari ya Mtakatifu Petero na kisha chuo kikuu cha upili cha Moi.

Baadhi ya vitu anavyovienzi mtanashati huyu ni;
1) Burudani ya mziki, filamu za vita na za mahaba.
2) Kutangamana na watu hasa wa kufu yake kimawazo na vilevie wacheshi. Anaamini kuwa ucheshi ni dawa mujarabu na kiungo muhimu cha maisha.
3) Anathamini sana kuwa nadhifu kila wakati na kuvutia.
4) Kuvinjari mtandao mara kwa Mara. Hasa sana, facebook, WhatsApp, LinkedIn, Twitter na baruapepe (email)

Anangwe hapendi vitu vifuatavyo,
1) Watu wambea
2) Watu wasio waaminifu
3) Kufanya vitu kwa minajili ya kuwafurahisha watu

Vyakula anavyovienzi ni;
1) Minofu kama vile ya kuku
2) Mboga za majani za kiasili kama vile mrenda, mitoo, managu, saga na eshitianyi (maharagwe yaliyopondwa)
3) Mayai ya kukaanga na mkate wa boflo kwa chai kama kisebeho
4) Sima [ati kwa sababu anazo jeni(genes) za kibaluhya😀]

Mwana wa watu huyu hashabikii chipsi na ndizi za kutokosa.

Victor anapenda rangi ya samawati. Si sare ya shule ya msingi alikosomea, si sare ya shule ya upili, si vilabu vya Chelsea na AFC leopards anavyoshabikia…. Buluu inashamiri kote kote. Hata katika taaluma ya kubuni michoro (graphic designing), huondokea kuitumia rangi hii ya samawati. Vile vile, anaipenda rangi nyeupe.

Hii hapa mitandao yake ya kijamii;
Facebook ~ Joshwa Victor Anangwe
Twitter ~ Hon. Anangwe
LinkedIn ~ Victor Anangwe

Instagram ~ Joshwa Victor

Je, unataka tutoe maelezo kukuhusu ili upate kujielewa vizuri, ufahamike vyema kwa rafiki zako, kuweka kumbukumbu mtandaoni na kupata rafiki wengine? Nitumie ujumbe kwenye:

 • 254729673536

ama

 • hussaynqassym@gmail.com

Shukrani za dhati kwa kusoma!

©husni

KUNUNUA MBARI

Na Mturi Katana,

Mila na Tamaduni ya Wagiriama

Wageni wanaokuja huku kwetu na wanataka kuishi nasi huwa wanaruhusiwa kununua mbari ili waingie katika mila na tamaduni zetu.

Huwa kuna sherehe ya wageni kuingizwa katika mbari zetu. Na wanaacha majina yote ya kwao na kupewa majina mapya. Ila wataitwa Mbari hio na kuongezwa neno wageni

Kama ni wa Milulu wataitwa

Wamilulu-Wageni

Kama ni wa Mwathoya wataitwa

Wamwathoya-Wageni

Kuashiria kwamba walinunua mbari
Kununua Mbari huwa kuna taratibu zifatazo;

1. Kuoshwa/Cleansing

Tambiko la kuwatowa laana na mikosi wageni ili waweze kuishi vizuri na kutangamana na wenyeji.

2. Kuweka Maagano ya Kuishi Pamoja

Hapa huwa kuna kuchinjwa kwa mfugo mwenye miguu minne kama vile mbuzi, ng’ombe na kadhalika. Damu humwagwa kuonyesha maagano ya wageni na wenyeji.

Katika maagano haya wageni huapa kwamba watafata mila na dasturi za wenyeji. Watajiunga na ‘dini‘ ya wenyeji.

3. Wazee wa Mbari

Wazee wote katika kijiji walio mbari hiyo huitwa ili kuendesha na kushuhudia wageni wanaojiunga na mbari hio. Huwa ni furaha kubwa maana mbari yao yaongezeka watu.

Baada ya sherehe hio wageni huingia rasmi katika mbari mpya.

Ila bado watakuwa na jina wageni. Baada ya vizazi kadhaa ndio watatambulika kama wenyeji.

MFAHAMU ESTHER

Ukimwita Esther Zighe, ataitika. Hasa sana, hupata raha isiyo kifani anapoitwa Zighe. Anawathamini watu wamwitao kwa jina hili lake la pili. Binti huyu ni mlimbwende wa kupitiliza. Haiba yake inaelea miongoni mwa huru laini, wale wa paradiso. Yuko kwenye majira ya machweo ya miaka ya ishirini na miwili. Ifikapo oktoba, tarehe tano mwaka huu,atakuwa ameongeza mwaka mmoja na busara.

Ngozi yake, maji ya kunde. Uzuri wa Esther haumhitaji sana kutia vipodozi kama vile wanja na podari. Ni banati mwenye kimo cha wastani, asiye mnene sana wala mwembamba sana. Anazienzi nywele zake za kiasili ambazo vilevile huchangia kuunga urembo wake. Aisee! Ni binti wa elfu.

Kwa sasa, ameufanya mtaa wa Sparki, jijini Mombasa, kuwa makaazi yake. Ni mwanafunzi wa mwaka wa nne katika chuo Kikuu cha Moi, bewa la Mombasa. Kozi anayoisomea huko ni shahada katika taaluma ya Usimamizi wa Biashara (Business Management).

Esther ni binti mnyamavu Sana, ila simaanishi kwamba hazungumzi kamwe. Aghalabu, hupenda kuwa pekee yake na kuisemezesha nafsi yake. Utulivu huu wake humsaidia kuwaza kwa upana na kujaribu kuuelewa ulimwengu na walimwengu. Kamwe, hapendi mtu wa kuyaingilia mambo yake kwa undani ama kujishengesha naye sana. Mrembo huyu hana pupa ya mambo.

Endapo ataamua kukata kimya chake, mtoto wa watu hupenda mazungumzo mapevu, mapana na ya kina. Hayashabikii maongezi ya juujuu, chapwa, yasiyojenga na yasiyo na mwelekeo.

Esther anawachukia watu wanafiki kwa dhati yake yote. Vile vile, hawapendi waongo maishani mwake. Huona afadhali aambiwe ukweli, japo mchungu.

Binti huyu ana imani iliyopanda vidato. Imani hii yake imemwelekeza kujitendea wema na kuwatendea wema walimwengu. Amefanya mazoea ya kusikiliza nyimbo za ibada kila alfajiri aamkapo na usiku kabla ya kulala. Sijakutaarifu pia kuwa ni mwimbaji hodari. Anaposhindwa kumwauni aliye na tatizo, hukereka sana akajilaumu na kujiona duni.

Esther anapenda watu wanyenyekevu na wastaarabu. Anathamini sana uadilifu na uaminifu. Vile vile, hupenda kupata rafiki wapya wa kumheshimu na kumthamini.

Ghashi Zighe huwa na mihemko na jadhba za hisia ambazo mara nyingi humfanya kuchachawa. Hivyo basi, huwa bora rafikize wakimfahamu na kumwelewa hivyo. Aghalabu, huwa mpungufu wa subira, hasa inapohusu kumngoja mtu waliyeahidiana kupatana. Esther huchunga Sana muda na huyafanya mambo yake kwa wakati na kufuata ratiba ya bongo lake. Abadan, hapendi miziki yenye mahadhi ya juu na hupenda kukaa chumbani anapokuwa hana shughuli za urasimu kama kwenda skuli.

Esther anaipenda familia yake kwa dhati.

Hivi hapa baadhi ya vyakula anavyovienzi dada huyu;
1) Kuku wa kuchomwa kwenye mafuta
2) Sima kwa samaki
3) Chai
4) Machungwa na matikiti maji.
Hapendi anapoandaliwa sima kwa mboga za majani kama vile mchicha, mkunde, mlenda na kadhalika.

Hofu alizo nazo ni;
1) Vurugu, unyanyasaji, ghasia na ukatili
2) Kujiingiza kwenye mahusiano yasiyofaa
3) Woga wa maji makuu kama vile bahari na urefu sana kama kuwa ghorofani
4) Jongoo (millipedes)
5) Uchungu wa namna yoyote

Hapendi ndizi na maparachichi kwa sababu ya ladha yake japo hujibidiisha kula, hasa inapojuzu sana.

Mlimbwende huyu anaikumbatia rangi ya samawati. Anaipenda kwa kuwa humpa furaha na amani.

Je, unataka tutoe maelezo kukuhusu ili upate kujielewa vizuri, ufahamike vyema kwa rafiki zako, kuweka kumbukumbu mtandaoni na kupata rafiki wengine? Nitumie ujumbe kwenye:

 • 254729673536

ama

 • hussaynqassym@gmail.com

Shukrani za dhati kwa kusoma!

©husni

MORO

Na Masito Ali,

Huu ni utamaduni wa jamii ya kidigo hususan wasichana wanawali .
Wanawali Hawa walikuwa wakikusanyana mahali walipopateuwa usiku wa kuanzia saa tatu au nne yaani baada ya kula chakula chao cha jioni
Ilikuwa wanakusanyika na kuimba kwa shangwe na vigelegele na dhumuni haswa wa tamaduni hii ilikuwa kusaka wachumba..

Wangeimba nyimbo zikavutia na hapo Basi mashabab wakiwa wanawatizama na kuwasikiliza.
Endapo barobaro nae angependezewa na mmoja Kati ya wanawali wale Basi angeenda na kumgusa bega Kisha msichana akamuanda na kumwambia “ikiwa kweli wanitaka tuma watu wako Mimi kwetu Ni familia ya mzee fulani”…

Na endapo utamgusa bega na asikufuate ujuwe hakukupenda .
Tamaduni hii ilileta uwiano na maadili mema ukilinganisha na utovu wa adabu uliopo hivi Sasa kwa kukosekanwa kwa tamaduni Kama hizi

Tamaduni hii ilidumisha ndoa,vile vile mimba za mapema hazikupatikana kwa wingi Kama zilivyo Sasa..
Wadigoooooo ipo haja tufufuweni tamaduni zetu nyingi zilizosahauliwa!

Courtesy of Value Based Education
Cc Sambasport Youth Agenda
Cc Aga Khan Foundation

MFAHAMU FAITH

Jina lake ni Faith N Mwandah. Huona heri kuyatumia majina yake mawili; la kwanza na la mwisho. Hulisaza hilo la Kati isipokuwa kwenye shughuli rasmi, tena inapolazimu sana. Ni binti ambaye amefaidi uhai kwa miaka ishirini na mitano sasa.

Faith ni binti mrembo na ambaye anapenda kutangamana na watu na hufanya usuhuba na yeyote. Unyonge alio nao ni kuwa huwatakia furaha rafiki zake na yeyote wa karibu kwake. Hufanya hivi hata inapobidi kujikwaza yeye binafsi na kujikosesha amani.

Rangi ya ngozi yake ni hudhurungi hafifu. Kimo chake, futi tano nukta sita (5.6). Faith amejaaliwa miguu yenye afya sana na ambayo humtatiza kupata sitara ya maguu yake. Wakati wa kununua viatu sokoni ama dukani, huelekea kuwamakisha wauzaji wa bidhaa hii adhimu kwa huo ukubwa wa viatu anavyohitaji. Nambari nane hufana kwake. Japo huu ni ukubwa uliopitiliza kwa mtoto wa kike, maguu haya yenye siha husaidia kuunga urembo wake.

Kwa muda mrefu sana, alikuwa ashiki wa kuzinyoa nywele zake kila ilipohitajika, ila kwa sasa, ameubadili mkondo wa mambo. Anafuga rasta kwa sasa na ana imani kuwa zitaongezeka na kuwa ndefu kuafiki matarajio yake.

Si mwembamba Sana wala si mnene wa kupindukia. Rafiki zake humchukulia kuwa kifyefye, mtazamo asioona kuwa na mashiko yoyote. Kwa kifupi, ni wa wastani tu. Faith hana michoro ya mwilini (tatoos) na wala hatarajii kujishengesha na hili. Kwenye mwili wake, lipo kovu moja tu alilopata udogoni, ambalo ni kikumbusho cha usumbufu wake alipokuwa bado kikembe.

Anasakini Mombasa kwa sasa ila huwa na ziara za mara kwa mara za kikazi ambazo humfikisha miji ya Nairobi na Nakuru.

Binti huyu ni mwanafunzi katika chuo kikuu cha kiufundi cha Mombasa. Huko, ameivalia njuga shahada katika taaluma ya Uhandisi, tawi la elektroniki (Electrical Engineering). Kando na masuala ya shuleni, Faith amejitosa kwenye tasnia ya uandishi wa fasihi katika lugha ya kiingereza. Blogu yake ya binafsi ambamo hufanya machapisho yake ni, http://mwandahspeaks.wordpress.com

Vile vile, ni mshairi kwenye tovuti,
http://Rapando.co.ke

Isitoshe, ni mwanachama wa vuguvugu la waandishi wa Mombasa (Writers Guild Mombasa chapter).

Faith anapenda sana kusoma vitabu kando na uandishi wake. Mara nyingi, huishia kusoma nakala laini za vitabu akitumia rununu yake yenye kiwambo kipana na ambayo huhifadhi nishati kwa muda mrefu. Simu hii humfanikishia sana usomaji wake.

Yeye ni mtu wa ndani kwa ndani. Hupenda kukaa chumbani anaponafasika. Kasumba hii yake imempa uraibu wa Kutazama sana filamu ila hili halimzuilii kutangamana na rafikize na kuuvinjari ulimwengu.

Vile vile, ni ashiki mkubwa wa kusafiri, kuogelewa na kujifurahikia mwenyewe.

Binti Faith anawachukia sana watu wa kujivuna na ambao hujiona wajuaji wa kila jambo.

Miili ya wafu ndilo pigo kubwa kwa dada huyu. Kamwe hawezi kustahimili kuutazama mwili wa maiti. Sasa je akaja kupewa jukumu la kuosha ama kukafini maiti? Mazingira ya matanga na uwepo wa huzuni na simanzi pia humtatiza Faith. Huemewa si kidogo.

Mtoto wa watu anapenda sana kuku. Awe wa kuchemsha, wa kupaka ama kuchomwa, hula bila ya kuchagua. Hukifakamia kitoweo hiki asisaze hata mfupa. Bora zaidi, mwandalie sima kwa kuku! Hula akazidiwa. Kwake, hii ndiyo Paradiso yake ya hapa duniani. Hupenda pia kula vyakula vya barabarani kama vile shawarma, samosa, mtura, pizza za kiswahili na kadhalika.

Hapendi maboga (pumpkins), nduma na mikate ya kuokwa (boflo). Huwa radhi kushinda njaa ama aandae chakula kingine.

Anaienzi rangi ya samawati kwa kuwa ni rangi iliyotulia, yenye amani na ambayo huashiria furaha.

Bila ya kusahau, Faith ni shabiki sugu wa soka. Vile vile, ni hodari wa kusakata kabumbu ya mdomo akawapiku mahiri wa fani hii. Kilabu anachoshabikia ni Arsenal ya Uingereza.

MFAHAMU RONNY

Mwite Ronny Odhiambo. Ghulamu bashashi sana asiye mchoyo wa tabasamu lake. Kando na kutokuwa mchoyo wa tabasamu, Ronny vile vile hamnyimi mtu yeyote aliye na uhitaji na pia asiyekuwa na uhitaji. Maadamu anacho, huona fahari kubwa kugawana na wenzake, kiwe kingi ama kidogo, ili wafaidi na kufurahi pamoja. Nyakati zingine, hugawa akajisahau maskini mtoto wa watu.

Ngozi yake imekoleza rangi ya hudhurungi. Ni mzuri wa sura na tabia vile vile. Maguu yake huhitari sana viatu vya kusetiri kotekote badala ya malapa ambayo huelekea kuyatumia tu anapoenda bafuni kukoga. Nambari ya viatu vinavyomtosha barabara ni arobanne na mbili (42). Nazo suruali zinazomkaa vizuri kiunoni huwa za upana wa sentimita thelathini na moja (31). Kimo chake ni cha wastani.

Anaponyoa, mwana wa watu huondoa dalili zote za nywele, kichwa kikabaki safi. Mara moja moja, huhiari kuzifuga nywele zake akalazimika kuzichana kila inapojuzu.

Hupenda Sana kukosolewa kinaganaga kila anapokosea. Ronny si mwepesi wa kuhamaki ila kero inapomfika pomoni, hutenda ubaya, akaishia kujilaumu. Awapo kwenye ulingo wa mahaba na mpenzi, dume Ronny anakiri kuwa huwa mwingi wa wivu. Hupenda kukifaidi chungu chake cha asali peke yake, akawa radhi kukilinda kwa vyovyote vile dhidi ya midomo mingine.

Ronny ana roho ya huruma sana hasa kwa adinasi wenye matatizo na waliokwazika maishani. Hujibidiisha kadiri ya uwezo wake kuwatilia pondo hao wenye shida. Hili humpa kitulizo murua na furaha.

Kwa sasa, makazi yake ni mtaa wa Sparki, jijini Mombasa. Amehitimu na shahada katika taaluma ya Afya ya Jamii katika chuo Kikuu cha kiufundi cha Mombasa.

Hupenda sana kutangamana na rafikize wakapiga gumzo na kulitowelea na vicheko sufufu. Vile vile, Ronny anao uraibu wa kutafuta na kuvumbua mambo mapya kutoka vitabuni. Kulingana naye, vitabu vimesheheni siri zote za maisha na ulimwengu. Kwake, vitabu ni kiungo muhimu Sana katika maisha yake, sawia na mipasho ya habari za kila siku. Vichekesho navyo huchangia pakubwa kuukamilisha utu wake na kuziremba siku zake.

Baadhi ya vitu anavyovchukia mtanashati huyu ni;
1) Watu washindani sana na wabishi
2) Mapuuza
3) Ukosefu wa heshima
4) Mwendo shaghalabaghala wa maisha

Vyakula avipendavyo Ronny ni;
1) Chapati za kutowelea na mchuzi mzito wa rojo ya karoti na upuzi mwingine
2) Sima iliyoiva kisawasawa. Hasa iliyoivishwa na moto wa jiko la makaa
3) Tende, ndizi na maparachichi

Hapendi kula nyama, mapapai na vyakula vilivyopikwa kutumia mafuta ya aina ya ‘margarine’. Anadai kuwa hawezi kustahimili harufu ya mafuta haya na vile vile, yanapotumiwa kupika, huua virutubishi kwenye chakula. Nalo papai humfanyia uchachu mdomoni na humtapisha anapolila.

Rangi anayoipenda na kuikumbatia kwa dhati ni ya nili ( buluu iliyokoza). Kwake, rangi hii huashiria uwepo wa sheria za Mwenyezi Mungu. Vile vile, hupendeza ajabu anapovaa nguo za rangi hii.

Je, unataka tutoe maelezo kukuhusu ili upate kujielewa vizuri, ufahamike vyema kwa rafiki zako, kuweka kumbukumbu mtandaoni na kupata rafiki wengine? Nitumie ujumbe kwenye:

 • 254729673536

ama

 • hussaynqassym@gmail.com

Shukrani za dhati kwa kusoma!

©husni